Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, Mohammad Baqer Zolqadr, amesema kuwa Mlango wa Hormuz hautafunguliwa hadi Marekani itakaporekebisha mwenendo wake, akisisitiza kuwa Iran haitatoa makubaliano yoyote katika suala hilo.
Zolqadr ameyasema hayo katika ujumbe wake alioutoa kwa maadhimisho ya Siku ya Wanahabari nchini Iran, ambapo aliwapongeza waandishi wa habari na wanahabari wanaofanya kazi katika uwanja wa habari, uhamasishaji na uelimishaji wa umma.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Iran IRNA, Zolqadr amesema kuwa kurekebisha mwenendo wa Marekani kunamaanisha mambo yafuatayo:
Kuacha kuitishia Iran kwa namna yoyote au kwa lugha yoyote, pamoja na kuacha kudhalilisha matukufu ya wananchi wa Iran.
Kukomesha kabisa vita na mashambulizi yake dhidi ya Iran, pamoja na mashambulizi dhidi ya washirika wa Iran nchini Lebanon, Palestina, Yemen na Iraq.
Kuondoa kizuizi cha baharini na kuondoa vikosi vyake vya kijeshi, vya majini na anga, kutoka maeneo yanayoizunguka Iran.
Kulipa kikamilifu fidia ya uharibifu uliosababishwa na vita viwili vya uchokozi vilivyolazimishwa dhidi ya Iran.
Kuondoa vikwazo visivyo vya haki na visivyo halali vilivyowekwa dhidi ya wananchi wa Iran.
Kufungua bila masharti fedha za wananchi wa Iran Zilizozuiliwa na, kwa mujibu wa taarifa hiyo, kuchukuliwa kinyume cha sheria.
Zolqadr amesisitiza kuwa hayo ndiyo madai ya wananchi wa Iran ambayo wamekuwa wakiyapaza sauti kwa muda wa siku 160 za uwepo wao mfululizo katika mikusanyiko ya hadhara.
Aidha, amesema kuwa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran halitatoa makubaliano yoyote, iwe katika uwanja wa vita au katika mazungumzo, akisisitiza msimamo mkali wa Iran kuhusu masharti ya kufunguliwa kwa Mlango wa Hormuz.
Maoni yako